Skip to main content

Udhibiti wa malaria uko katika hatihati baada ya dawa kuwa sugu:WHO

Udhibiti wa malaria uko katika hatihati baada ya dawa kuwa sugu:WHO

Juhudi za kimataifa za kudhibiti malaria huenda zikakabiliwa na pigo kubwa kama hatua madhubuti hazitochukuliwa kuzuia usugu wa vijidudu vya ugonjwa huo dhidi ya dawa iliyopo ambayo imekuwa muhimu katika kupambana na malaria.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO dawa ya artemisinin hadi sasa imekuwa ni silaha muhimu ya kukabili malaria na kuwa sugu kushindwa kutibu tena itakuwa zahma kubwa katika vita vya ugonjwa huo. Maeneo ya mpakani mwa Cambodia na Thailand tayari yameripoti usugu dhidi ya artemisinin.

Akizindua mpango wa kukabiliana na usugu dhidi ya dawa ya artemisinin mkurugenzi mkuu wa WHO Margaret Chan amesema , kushindwa kufanya kazi vizuri kwa dawa hiyo kutasababisha ongezeko kubwa la vifo vya malaria. Amesema mpango waliozindua utatoa fursa ya kuangalia historia ya udhibiti wa malaria na kuzuia chanzo cha usugu dhidi ya dawa hiyo na usisambae zaidi. Katika muongo uliopita WHO inakadiria kwamba visa vya malaria vimepungua kwa zaidi ya asilimia 50 katika nchi 43.