Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waathirika wa mafuriko Sri Lanka wapata msaada

Waathirika wa mafuriko Sri Lanka wapata msaada

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa limeanza kutoa misaada kwa serikali ya Sri Lanka ili kusaidia watu zaidi 330,000 wanaohitaji msaada wa dharura baada ya kuathiriwa na mafuriko yaliyoikumba wilaya ya Ampara.

Watu zaidi ya 28,000 wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani na baadhi yao kulazimika kuishi kwenye majengo ya shule kufuatia makazi yao kusombwa na mafuriko. Kundi jingine la watu wanaokadiria kufikia 26,000 wanapatiwa hifadhi kwa ndugu na jamaa zao kwani makazi yao pia yameharibiwa na mafuriko hayo.

Shirika hilo la umoja wa mataifa IOM ambalo linafanya kazi na taasisi ya taifa ya kukabili majanga ya Sri Lanka, limekuwa likiwahudumia wananchi hao hasa wale waliko katika maeneo ambayo mafuriko hayo yameleta maafa makubwa.

Makambi mbalimbali yameanza kujengwa kwa ajili ya kuwahifadhi waathirika hao na tayari misaada ya dharura kama mablanketi, maziwa pamoja na vifaa vingine kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kilimo imeanza kuwafikia wananchi hao.