Mkuu wa haki za binadamu alaani mauji ya kidini duniani kote

Mkuu wa haki za binadamu alaani mauji ya kidini duniani kote

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay leo amelaani mashambulio ya karibuni yanayolenga makundi ya kidini katika nchi mbalimbali duniani.

Ameyataka mataifa kuonyesha nia ya kupambana na ghasia za aiana hiyo na kufuta sheria za kibaguzi na mila zinazoathiri makundi machache ya kidini katika jamii.

Amesema mashambulizi ya karibuni yamekatili maisha ya watu wengi kwenye nchi kadhaa na yamekuwa yakifanywa na makundi ya walio na itikadi kali hali inayoashiria kuongezeka kwa ubaguzi wa kidini na kuzidisha hofu.

 Bi Pillay amesema anaamini kuna hatua zinazoweza kuchukuliwa kusaidia kuchagiza kuvumiliana katika masuala ya dini na kupunguza mashambulio ya aina hiyo.

Pia amepongeza hatua ya kulaaniwa kwa mashambulizi ya Misri nakulikofanywa na viongozi wa dini, makundi ya kidini, viongozi wa siasa na wa jumuiya za kiraia na hata vyombo vya habari baada ya shambulio la bomu katika kanisa la Coptic mjini Alexandria siku ya mwaka mpya.

Amesema mashambulio katika makanisa, misikiti, masinagogi, mahekalu na maeneo mengine ya kidini duniani kote ni kama kengele ya kutuamsha sote kupambana na uasi huo. Mwaka 2010 mamia ya watu wameuawa katika mfumo huo ikiwepo Nigeria, Misri, Iraq, Pakistan, Malasyia na Indonesia.