Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya Wasudan Kusini warejea nyumbani kupiga kura

Maelfu ya Wasudan Kusini warejea nyumbani kupiga kura

Mamilioni ya raia wa Sudan Kusini wanajiandaa kupiga kura ya maoni ya kihistoria Jumapili Januari 9 ili kuamua uhuru wa eneo lao.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linasema idadi ya raia wa Sudan Kusini wanaorejea nyumbani kwa ajili ya kupiga kura kutoka Kaskazini imeongezeka mara mbili tangu Desemba mwaka jana na sasa wamefikia 120,000.

Kwa mujibu wa shirika hilo watu 2000 wanavuka kila siku kuingia Sudan Kusini na wengine wengi wanatarajiwa kuwasili kabla ya Jumapili. Hata hivyo kuna hofu imeenza kujitokeza kuhusu Wasudan Kusini walioko Kaskazini ambao watashindwa kurejea nyumbani. Melissa Fleming ni msemaji wa UNHCR

(SAUTI YA MELISA FLEMING)

Wasudan Kusini wapitao milioni 4 wanatarajiwa kupiga kura siku ya Jumapili kuamua endapo wawe taifa huru na kujitenga na Kaskazini na kuwa taifa la 54 la Afrika ama la.Nalo jopo la watu watatu lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuangalia kura hiyo tayari lipo Sudan tangu mwanzoni mwa wiki likiongozwa na Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa na litazunguka nchi nzima kuangalia upigaji kura, kuhesabu na kutangazwa matokeo kwa awamu. Kura hiyo inapigwa kwa muda wa wiki moja hadi Januari 15.