Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yamkumbuka msanii wa Msumbiji Malangatana

UNESCO yamkumbuka msanii wa Msumbiji Malangatana

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la sayansi elimu na utamaduni UNESCO leo ametoa salamu zake za rambirambi na heshima ya kumkumbuka msanii maarufu wa Msumbiji ambaye pia alikuwa msanii wa amani wa UNESCO Valente Ngwenya Mulangatana aliyefariki dunia jana Jumatano.

Bi Irina Bokova amesema kwa kifo cha Malangatana , sanaa ya afrika imepata pigo kubwa, kwa kupoteza mmoja wa watu wenye vipaji. Ameongeza kuwa hakuwa tuu msanii bora bali pia mpigania amani mkubwa.

Malangatana alizaliwa katika kijiji cha Matalanga Kusini mwa Msumbiji mwaka 1936 na alifahamika sana kwa uchoraji wake wa kwa kutumia vitambaa vya canvas, pia kuchonga, kuweka nakshi, ufinyanzi, na ushairi.

Baada ya uhuru mwaka 1975 Malangatana alipata kazi ya masuala mengi ya umma ikiwemo kuchora picha katika makavazi ya historia ya nchi hiyo na kitivo cha elimu ya masuala ya Afrika kwenye chuo kikuu cha Eduardo Mondlane. Mwaka 1997 Malangatana alipamba Maputo wakati wa mkutano wa UNESCO wa utamaduni kwa ajili ya sanaa na ndiopo mwaka huohuo akachaguliwa na UNESCO kuwa msanii wake kwa ajili ya amani.

Moja ya kazi zake ni picha maalumu ya vijana na amani ambaye imewekwa kwenye makao makuu ya UNESCO mjini Paris.Na pia waweza kuona sanaa zake kwenye makavazi ya taifa na vituo binafsi vya sanaa katika nchi mbalimbali ikiwemo Angola, India, Nigeria, Ureno na Zimbabwe. Ni mmoja kati ya wasanii mbalimbali ambao ni wa amani wa UNESCo akiwemo mwanamuziki nyota wa Cameroon Manu Dibango.