Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi Sri Lanka wataka kurejea nyumbani: UNHCR

Wakimbizi Sri Lanka wataka kurejea nyumbani: UNHCR

Idadi ya wakimbizi wa Sri Lanka wanaotaka kurejea nyumbani tangu kumalizika kwa vita mwaka 2009 inaongezeka limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Maelfu ya watu nchini humo walikimbia kwa sababu ya muongo wa vita kati ya majeshi ya serikali na Liberation Tigers of Tamil eelam LTTE, ambao wamekuwa wakipigania uhuru wa eneo la Tamil.

Jennifer Pagonis naibu mwakilishi wa UNHCR mjini Colombo amesema wengi wa wakimbizi hao wamekuwa nje ya nchi kwa miaka mingi na sasa wako tayari kurejea nyumbani. Mwaka jana idadi ya wakimbizi waliorejea nyumbani ilikuwa 2054 ikilinganishwa na 843 ya 2009, na wengi wao wanaotoka katika kambi ya wakimbizi ya Tamil Nadu nchini India

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali ya India kuanzia tarehe mosi Novemba 2010 wakimbizi wa Sri Lanka zaidi ya 70,000 wanaishi katika makambi 112 Tamil Nadu na 32,467 wanaishi nje ya makambi nchini India. Jumla ya Wasri Lanka 146,098 wameandikishwa kama wakimbizi katika nchi 64 duniani.