Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfanyakazi wa UNAMID achiliwa Sudan baada ya siku 90

Mfanyakazi wa UNAMID achiliwa Sudan baada ya siku 90

Mfanyakazi wa mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika Darfur Sudan UNAMID ameachiliwa huru baada ya kushikiliwa mateka kwa siku 90.

Mfanyakazi huyo alittekwa kwenye maskani yake mjini el Fasher tarehe 7 Oktoba mwaka jana na ameachilia huru leo. Wakati wa tukio la kutekwa kwake wanajeshi watatu wa kulinda amani walitekwa pia na watu watatu wasiojulikana waliokuwa na silaha na walikimbia kwa kutumia gari la UNAMID lililokuwa limeegeshwa nje ya makazi yao.

Wawili kati ya mateka hao walifanikiwa kutoroka kutoka kwenye gari hilo. Mfanyakazi huyo ambaye ni raia wa Hungary aliachiliwa mchana wa leo na kusafirishwa na serikali ya Sudan hadi el Fasher ambako amefanyiwa uchunguzi wa afya.

Anaonekana kutodhuriwa na yuko kwenye afya nzuri na baada ya uchunguzi amepelekwa Khartoum. Mkuu wa UNAMID Ibrahim Gambari ameelezea hisia zake baada ya kuachiliwa mfanyakazi huyo na kusema tunashukuru kwa kumpata tena mfanyakazi mwenzetu akiwa salama na mwenye afya.

Kuachiliwa kwake kunafuatia juhudi za serikali ya Sudan ambayo imekuwa katika mawasiliano kwa muda wote na UNAMID, serikali ya Hungary pia imefahjamishwa na ilikuwa ikishirikiana na UNAMID na serikali ya Sudan kuhakikisha anaachiliwa kwa amani na usalama. Tangu kuanzishwa kwa UNAMID 2008 walinda amani 10 wa UNAMID wametekwa.