Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID inawalinda maelfu ya wakimbizi wa ndani Darfur

UNAMID inawalinda maelfu ya wakimbizi wa ndani Darfur

Mpango wa pamoja wa kulinda amani kwenye jimbo la Darfur wa Umoja wa Mataifa na muungano wa Afrika UNAMID unaimarisha uwepo wake kwenye jimbo hilo ili kuhakikisha usalama wa maelfu ya wakimbizi wa ndani.

Baada ya machafuko ya hivi karibuni baina ya vikosi vya serikali ya Sudan na waasi UNAMID leo imesema usalama katika maeneo yaliyoathirika ya Kaskazini na Kusini mwa Darfur umerejea kiasi, huku usafiri ukianza kama kawaida katika maeneo mbalimbali.

Msaada unaendelea kuwafikia maelfu ya wakimbizi wa ndani ambao wengi wao wametafuta hifadhi nje ya eneo la UNAMID. Mpango huo pia umesema unafuatilia taarifa za kuzuka mapigano ya kikabila kati ya jamii za Misseriya na Rizeigat Magharibi mwa Darfur.

Mapigano ya karibuni yalizuka December kati ya vikosi vya serikali na vya waasi wa Sudan liberation Army/ minni Minawi (SLA/MM) na kusababisha wimbi jipya la wakimbizi wa ndani.