Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa kisiasa Ivory Coast kuathiri mamilioni:UNICEF

Mgogoro wa kisiasa Ivory Coast kuathiri mamilioni:UNICEF

Watu wanaokadiriwa kuwa milioni 2.4 huenda wakaathirika na machafuko ya kisiasa nchini Ivory Coast kwa mujibu wa mashirika ya kibinadamu Afrika ya Magharibi.

Idadi hiyo ni pamoja na watu 45,000 wanaotarajiwa kuwa wakimbizi wa ndani, na watu 150,000 watakaokimbilia nchi tano jirani za Liberia, Guinea, Mali, Burkina Faso na Ghana. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linasema Waivory Coast kati ya 20,000 na 25,000 wamekimbilia nchi jirani huku asilimia zaidi ya 75 ni wanawake na watoto.

Shirika hilo linasema litahitaji dola milioni 20 ili kukabiiana na mahitaji ya watoto na wanawake walioathirika na machafuko ya baada ya uchaguzi nchini Ivory Coast na nchi jirani. Mahitaji kama maji safi, malazi na chakula ndio makubwa kwa wakimbizi wa ndani, wakimbizi wengine na familia zinazowahifadhi ikiwa ni pamoja na ulinzi, afya na elimu.

UNICEF inasema mahitaji hayo ni muhimu kupinguza hatari ya kuhara, kipindupindu na magonjwa mengine yatokanayo na maji kwa watu 182,000 ambapo 50,000 watakuwa makambini na 132,000 kwa fmilia zinazowahifadhi.