Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais Bashir atishia kujitoa kwenye mazungumzo na JEM

Rais Bashir atishia kujitoa kwenye mazungumzo na JEM

Rais Omar al Bashir wa Sudan amesema serikali yake itajitoa kwenye mazungumzo na kundi la waasi wa Magharibi mwa Darfur endapo hakunakuwa na muafaka ifikapo mwisho ya siku ya leo Alhamisi Desemba 30.

Wapatanishi wa mazungumzo hayo ya Qatar sasa wanafanya majadiliano na wawakilishi kutoka pande zote. Rais Bashir ametishia kuyapeleka mazungumzo hayo Darfur na kukabiliana na yeyote atakayekamata silaha.

Waasi hao wa kundi la Justice and Equality Movement JEM wamekuwa wakipambana na majeshi ya serikali na wanamgambo wa Kiarabu wanaodaiwa kuiunga mkono serikali.

Bashir akizungumza mbele ya umati wa watu mjini Darfur amesema endapo hakuna muafaka wowote hadi mwisho wa siku ya leo wataondoa watu wao kwenye mazungumzo hayo.

(SAUTI YA OMAR AL-BASHIR)

Kundi la JEM ambalo limeelezwa kuwa na silaha lukuki limekataa kutekeleza tamko hilo la Rais Bashir na kusema hotuba yake ilikuwa ni kutangaza vita. Bwana Bashir anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC inayomshutumu kwa makosa ya uhalifu wa vita na mauaji ya kimbari kwenye jimbo la Darfur madai ambayo ameyakanusha vikali.