Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Balozi mpya wa Ivory Coast awasilisha hati huku wananchi wakitakiwa kudumisha utulivu

Balozi mpya wa Ivory Coast awasilisha hati huku wananchi wakitakiwa kudumisha utulivu

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Ivory Coast UNOCI imetoa ombi kwa watu wa Ivory Coast kuchangia katika juhudi za amani kwa kuwaruhusu walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutekeleza wajibu wao.

Nchi hiyo inakabiliwa na mtihani mkubwa wa kisiasa baada ya Rais Laurent Gbagbo kugoma kuyakubali matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwezi uliopita ambapo mgombea wa upinzani Alassane Ouattara alitangazwa mshindi. Hamadoun Toure ni msemaji wa UNOCI

(SAUTI YA HAMADOUN TOURE)

"Tunachotaka kufanya zaidi ya yote ni kuomba raia wasisiahau jukumu letu. UNOCI haiko katika vita na watu, hatuko katika vita na mtu yeyote. Tumekuja hapa kuwasaidia watu wa Ivory Coast kupata amani. Ni muhimu watu wawe tayari kuisaidia UNOCI ili iwasaidie."

Wakati huohuo hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa balozi mpya wa Ivory Coast Dr Youssouf Bamba amewasilisha hati zake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon. Balozi huyo amesema ni heshima kubwa kuteuliwa na Rais Alassane Ouatara kuiwakilisha nchi yake.

(SAUTI YA YOUSSOUF BAMBA)

Bwana Bamba amesema anamuunga mkono Alassane Uoattara na anaamini ndiye aliyechaguliwa kama Rais wa Ivory Coast.

(SAUTI YA BAMBA)

"Kwa sababu amechaguliwa katika uchaguzi, huru, wa haki, wazi na wa kidemokrasia. Matokeo yametangazwa na tume huru ya uchaguzi na kuthibitishwa na Umoja wa Mataifa kwa kuzingatia azimio la Pretoria na la Umoja wa Mataifa namba 1765, hivyo hakuna shaka juu ya hilo. Kwangu mjadala umekwisha, sasa tunachozungumzia ni vipi na lini bwana Gbagbo ataondoka madarakani."