Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa ndani nje ya makao ya UNAMID waendelea kupokea msaada

Wakimbizi wa ndani nje ya makao ya UNAMID waendelea kupokea msaada

Msaada unaendelea kuwafikiwa maelfu ya wakimbizi wa ndani walioko katika kambi ya muda nje ya makao ya mpango wa Umoja wa Mataifa na wa Afrika wa kulinda amani Darfur UNAMID eneo la Kaskazini na Kusini mwa Darfur.

Hata hivyo ugawaji wa msaada kwenye eneo la Shangil Tobaya Kaskazini mwa Darfur umesitishwa leo baada ya kutangazwa vikwazo vya kusafiri toka eneo moja hadi jingine.

UNAMID inashirikiana na maafisa wa usalama wa eneo hilo ili kuweza kuyafikia maeneo yaliyoathirika na mapigano na kuwapelekea msaada unaohitajika kwa njia iliyo salama.

UNAMID pia inachunguza taarifa za kuzuka mapigano katika eneo la Kazanjadeed yapata kilometa 40 kutoka mji wa Shaeria ambayo yanadaiwa kusababisha wimbi lingine jipya la wakimbizi wa ndani. Wahusika katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam nje kidogo ya mji wa El-Fasher wamesema wakimbizi zaidi ya 100 wamewasili wengi wakiwa wanawake na watoto. Wengine 14 wameelekea Tobaya na 5000 kwenye maeneo ya UNAMID.