Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suluhu ya mzozo wa Ivory Coast bado ipo njia panda

Suluhu ya mzozo wa Ivory Coast bado ipo njia panda

Juhudi za karibuni za jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS kumaliza mzozo wa kisiasa nchini Ivory Coast zimeshindwa kuzaa matunda.

Marais wa tatu Yayi Boni wa Benin, Ernest Bai Koroma wa Sierra Leone na Pedro Pires wa Cape Verde waliowasili jana nchini Ivory Coast na kukutana na Alassane Ouattara anyetambulika kimataifa kuwa mshindi wa uchaguzi wa mwezi uliopita na Rais Laurent Gbagbo aliyegoma kuondoka madarakani imebidi waondoke baada ya kushindwa kumshawishi Gbagbo kuachia madaraka. Viongozi hao wamekwenda Nigeria kutoa taarifa kwa Rais Goodluck Jonathan ambaye mwenyekiti wa sasa wa ECOWAS na wamesema watarejea tena mjini Abijan wiki ijayo katika jaribio la pili la kumtaka Gbagbo kukabithi madaraka kwa bwana Ouattara.

Mvutano huo wa kisiasa umesababisha vifo zaidi ya 100 tangu ulipozuka mwezi Novemba mwaka huu na kuwafanya maelfu kufunga virago na kukimbilia nchi jirani wakihofia usalama wao.