Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya lishe ya watoto nchini Niger bado ni ya kutia mashaka:UM

Hali ya lishe ya watoto nchini Niger bado ni ya kutia mashaka:UM

Ingawa misaada ya kibinadamu nchini Niger imeokoa maisha ya maelfu ya watoto wagonjwa, hali ya lishe bado inatia mashaka, ikiwa watoto 15 kati watoto 100 wanakabiliwa na utapia mlo uliokithiri.

Takwimu hizo zimetolewa na utafiti mpya wa Umoja wa Mataifa ukisema kwamba hofu inaendelea licha ya mavuno mazuri mwishoni mwa mwaka huu. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, shirika la mpango wa chakula duniani WFP na serikali ya Niger sasa wameitolea wito jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi na kutumia kila njia kupambana na utapia mlo nchini humo na chanzo chake. George Njogopa na taarifa kamili.

(SAUTI YA GEORGE NJOGOPA)

Jumuiya ya kimataifa imefanikiwa kuwafikia maelfu ya watoto nchini Niger ambao walikuwa hatarini kukubwa na matatizo ya utapiamlo,kutokana na ukosefu wa chakula unaendelea kulikumba eneo hilo.

Mwakilishi mkazi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na watoto UNICEF Guido Cornale amesema kuwa makundi yanayohusika na huduma ya usamaria mwema pamoja na wahisani wengine wamefanikiwa kukusanya nguvu na kusambaza chakula kwa watoto hao. 

Watoto wengi wamekuwa wakijitokeza kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kupata chakula pamoja na matibabu ya kiafya. UNICEF imesema kuwa bado chakula zaidi kinahitajika kwa ajili ya kuwafikia watoto wengi zaidi.

Ripoti za hivi karibuni zimeonya kuwa kumekuwa na mafanikio kiasi katika upunguzaji wa kiwango cha cha watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanakubwa na utapiamlo katika nchi za afrika magharibi.

Hata hivyo hali bado ni mbaya kwa watoto walio na umri wa miezi 6 hadi 23.