Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada waanza tena kuwafikiwa wakimbizi wa ndani Darfur:UM

Msaada waanza tena kuwafikiwa wakimbizi wa ndani Darfur:UM

Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada leo wameanza kupeleka msaada muhimu wa kibinadamu kwa wakimbizi wa ndani wanaohifadhiwa nje ya eneo la mpango wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika Darfur UNAMID baada ya kuondolewa vikwazo vyote vya usafiri wa anga na barabara kwenye maeneo yaliyoghubikwa na machafuko karibuni.

UNAMID ilisindikiza msafara wa malori manane hadi mjini Khor Abeche , kilometa 80 Kaskazini mashariki mwa Darfur Kusini mji mkuu wa Nyala ambako hivi karibuni kulishuhudiwa mapigano baina ya majeshi ya serikali na waasi.

Tani 19 za chakula ziliwasili kwa njia ya anga jana kwa wakimbizi wa ndani zaidi ya 1000 walioko nje ya makao ya UNAMID. Wakati huohuo msafara uliobeba mafuta na chakula kwa ajili ya wakimbizi wa ndani wanaokadiriwa kufikia 5000 walioko Shangil Tobaya Kaskazini mwa Darfur umeondoka mjini El Fasher mapema leo.

Na msaada kama huo utakaowasilishwa UNAMID na mashirika mengine ya misaada katika maeneo ya Shaeria, Jaghara na Negaha unaandaliwa katika siku chache zijazo. Watu takriban 300,000 wameuawa na wengine wapatao milioni 2.7 wamelazimika kuzikimbia nyumba zao tangu kuzuka kwa machafuko.