UNHCR inasema Thailand inawatimuwa wakimbizi wa Myanmar

28 Disemba 2010

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema serikali ya Thailand imewarejesha kwa nguvu nyumbani wakimbizi 166 wa Myanmar.

Wakimbizi hao ambao walilazimishwa kurejea nyumbani siku ya Jumamosi Desemba 25, walivuka mpaka na kuingia Thailand mwezi Novemba mwaka huu wakikimbia mapigano baina ya majeshi ya serikali na makundi ya waasi.

UNHCR inasema kuwatimua kwa nguvu wakimbizi ni kinyume na sheria za kimataifa ambazo zinakataza kuwafukuza waomba hifadhi. Wakimbizi hao ambao ni pamoja na wanawake 50 na watoto 70 wameripotiwa kusema hawako tayari kurudi nyumbani kwa kuhofia usalama wao.

UNHCR imiomba serikali ya Thailand kuhakikisha kwamba kurejea nyumbani Myanmar kwa wakimbizi kunafanyika kwa hiyari, na pale tuu ambapo mazingira mazuri ya wanaorejea yatakuwepo, kuhakikisha usalama na kulinda utu wao.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud