Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi zaidi wa Ivory Coast waingia Liberia: UNHCR

Wakimbizi zaidi wa Ivory Coast waingia Liberia: UNHCR

Taarifa zinasema wakimbizi zaidi wa Ivory Coast wanamiminika nchini Liberia wakihofia usalama wao kutokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR wakimbizi hao wengi wanaingia Mashariki mwa Liberia katika jimbo la Nimba. Hadi kufikia leo UNHCR inasema wakimbizi 15,120 wameorodheshwa kutoka vijiji vya Danane na Guiglo Magharibi mwa Ivory Coast na wengine 4000 wapya wamewasili Liberia.

Wengi wa wakimbizi hao ni wanawake na watoto khuku asilimia 62 ni wenye umri wa chini ya miaka 18. Wakimbizi hao ni mchanganyiko wa wafuasi wa Alassane Ouattara na Laurent Gbagbo, na wanasema wakmekimbia wakihofia kwamba mvutano huo wa kisiasa utasabisha tena vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ongezeko hilo la wakimbizi linatoa shinikizo kwa wenyeji wanaowahifadhi na kusababisha upungufu wa maji safi, chakula na malazi.

UNHCR inajitahidui kugawa msaada wa dharura wa vitu muhimu kwa vijiji 20 vinavyohifadhi wakimbizi ikiwemo matandiko ya kulalia, sabuni, maji, na chakula.