Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wazungumzia ghasia zinazoendelea jimbo la Darfur

UM wazungumzia ghasia zinazoendelea jimbo la Darfur

Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani kwenye jimbo la Darfur (UNAMID) kimeeleza hisia zake kunapoendelea kushuhudiwa mapigano kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na makundi ya waasi kwenye maeneo yanayokumbwa na ghasia.

UNAMID imetoa wito kwa pande zote kusitisha ghasia ambazo hazihatarishi tu maisha ya raia wasiokuwa na hatia bali pia zinavuruga mipango ya kutafuta amani. UNAMID imetoa wito kwa vikosi vya serikali na makundi ya waasi kuhakikisha usalama kwa makundi ya kutoa huduma za kibinadamu yanayowahudumia maelfu ya watu waliokimbia makwao baada ya mapigano ya juma lililopita.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon ameunga mkono jitihada zinazofanywa na UNAMID na mashirika ya Umoja wa Mataifa za kuwasaidia waathiriwa wa mapigano hayo akisema kuwa yote yanafanya kazi ngumu kuwakikishia usalama raia wanaoishi katika hali ngumu.