Wafuasi wa Ouattara waitisha mgomo Ivory Coast

Wafuasi wa Ouattara waitisha mgomo Ivory Coast

Wafuasi wanaomuunga mkono mshindi wa uchaguzi wa rais nchini Cote d\'Ivoire ambaye anatambuliwa kimataifa Allasane Ouattara wameitisha mgomo wa kitaifa nchini humo, kumlazimisha rais anayeng\'ang\'ania madarakani Laurent Gbagbo kuachia madaraka.

Iwapo mgomo huo utafanyika, utatokea kabla ya ziara iliyopangwa ya marais watatu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi, ECOWAS, kutembelea nchi hiyo. Ijumaa wiki iliyopita jumuiya hiyo ya ECOWAS ilimuonya bwana Gbagbo kutumia nguvu, iwapo haitopata ufumbuzi mwingine, kuweza kumuondoa madarakani, kwa niaba ya watu wa nchi hiyo.

Majeshi yanayomtii bwana Gbagbo bado yameendelea kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo Abidjan, huku serikali kivuli ya bwana Ouattara ikilindwa katika hoteli inakoendesha shughuli zake, na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wapatao 800.

Umoja wa Mataifa umearifu kuwa raia 14,000 wa Cote d'Ivoire wamekimbilia nchini Liberia, kufuatia ghasia zilizozuka baada ya duru ya pili ya uchaguzi nchini humo, msemaji wa Shirika la Kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR Fatoumata Lejeune-Kaba ametahadharisha kuongezeka kwa wakimbizi zaidi.