Skip to main content

Kubomolewa nyumba Jerusalem kwa laaniwa,UNRWA inasaidia familia

Kubomolewa nyumba Jerusalem kwa laaniwa,UNRWA inasaidia familia

Mkurugenzi wa Ukingo wa Magharibi wa mpango wa Umoja wa Mataifa wa msaada kwa Wapalestina UNRWA Barbara Shenstone leo amelaani ubomoaji wa nyumba mbili za wakimbizi Mashariki mwa Jerusalem.

Amesema kitendo hiki cha kulaaniwa kina athari kubwa, na ameitaka serikali ya Israel kusitisha shughuli za ubomoaji na kuwahamisha kwa nguvu watu katika maeneo yanayokaliwa ,kwani ni kinyume na wajibu wa Israel chini ya sheria za kimataifa ikiwemo mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za watoto ambao Israel umeuridhia.

Ameongeza kuwa wakati watoto kote duniani wanafurahia msimu wa sikukuu manyumbani kwao, watoto hawa wametaabika sana na kuathirika kwa kushuhudia nyumba zao zikibomolewa mbele ya wazazi wao.

Amesema kitendo hicho ni ukatili na cha kuchefua kwani familia hizo ambazo zililazimika kuwa wakimbizi wa ndani mwaka 1948, zinajikuta bila makazi tena.