Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vikosi vya AMISOM Somalia viongezwe:Baraza la usalama

Vikosi vya AMISOM Somalia viongezwe:Baraza la usalama

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limetoa wito wa kuongeza kwa asilimia 50 vikosi vya muungano wa Afrika vinavyolinda amani Somalia AMISOM. Baraza limetaka vikosi hivyo vinavyosaidia kurejesha amani na utulivu katika nchi iliyoghubikwa na machafuko kwa miaka 20 vifikie wanajeshi 12,000.

Katika kupitisha bila kupingwa azimio la kuongeza wanajeshi wa AMISOM hadi Septemba 30 mwaka 2011, wajumbe 15 wa baraza la usalama wamezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa kuchangia kwa hali na mali fedha na vifaa ili kuiwezesha AMISOM kutimiza wajibu wake ambao ni pamoja ya kurejesha amani na kuisaidia serikali ya mpito kuunda jeshi la usalama wa taiafa na la polisi .

Baraza limemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutoa msaada wa kiufundi na vifaa kwa jeshi hilo litakaloongezwa ili kukabiliana na wanamgambo wa Al Shabaab na wanamgambo wengine wa Kiislam, makundi yaliyogawanyika na wapiganaji kutoka nje wanaotaka kuing'oa serikalia ya mpito na kudhibiti eneo kubwa la Moghadishu.

Somalia haina serikali imara tangu kupinduliwa kwa utawala wa Siad Barre mwaka 1991, maelfu ya watu wameuawa na mamilioni kuwa wakimbizi wa ndani na nje tangu kuzuka kwa vita miongo miwili iliyopita.