Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapatanishi waitaka serikali ya Sudan na JEM kusitisha vita

Wapatanishi waitaka serikali ya Sudan na JEM kusitisha vita

Kundi la wapatanishi ukiwemo Umoja wa Mataifa linaloendesha juhudi za kupatikana kwa amani katika jimbo la Darfur limetoa wito kwa serikali ya Sudan na kundi la waasi wa JEM kuafikiana kusitisha mapigano kabla ya mwishoni mwa mwaka huu.

Kwenye ripoti iliyotolewa na wapatanishi hao wakiwemo Umoja wa Mataifa , Muungano wa afrika na serikali ya Qatar ni kuwa mazungumzo yaliyo na lengo la kusitisha mapigano yamerejelewa tena kati ya kundi la JEM na serikali kwenye mji mkuu wa Qatar Doha.

Mpatanishi mkuu kati ya pande hizo Djibril Bassolé amezitka kukamilisha mazungumzo kabla ya Disemba 31 na kujitolea kikamilifu kwenye mpango wa kutafuta amani. Takriban watu 300,000 wameuawa na wengine zaidi ya milioni 2.7 kulazimika kukimbia makwao tangu kuanza kwa ghasia katika jimbo la Darfur mwaka 2003 kati ya waasi na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na wanamgambo wa Janjaweed.