Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya Indonesia, Viongozi wa Dini na UNICEF kuchagiza unyonyeshaji

Serikali ya Indonesia, Viongozi wa Dini na UNICEF kuchagiza unyonyeshaji

Wakati serikali ya Indonesia ikiadhimisha siku ya kimataifa ya kina mama wiki hii, viongozi wa serikali, viongozi wa dini kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wameungana kuchagiza umuhimu wa kunyonyesha watoto.

Katika mkutano maalumu ulioandaliwa na wizara ya afya ya Indonesia kwa ushirikiano na wizara ya masuala ya dini, viongozi wa Kiislam, Kikristo, Kibudha, na Kihindu walijadili jukumu lao katika kuchagiza unyonyeshaji wa watoto. Akizungumza katika mkutano huo mwakilishi wa UNICEF nchini humo Angela Kearney amesema afya ya taifa inategemea mtazamo wa pamoja na hatua za pamoja zitakazochukuliwa na wadau wote.

Ameongeza kuwa suala la unyonyeshaji ni muhimu sana kwa afya ya mtoto hasa katika siku za mwanzo za maisha yake na kwa kuhusisha viongozi wa serikali na wa dini katika suala hilo ni muhimu sana.

Kiwango cha unyonyeshaji Indonesia kimepungua kwa asilimia 40 tangu mwaka 2002 na ni theluthi moja tuu ndio wanaonyonyesha watoto katika miezi sita ya mwanzo ambacho ni kiwango cha kimataifa.