Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa ndani wa Sudan Kusini wanaelekea nyumbani kupiga kura ya maoni

Wakimbizi wa ndani wa Sudan Kusini wanaelekea nyumbani kupiga kura ya maoni

Zaidi ya wakimbizi wa ndani 55,000 wa Sudan Kusini wamerejea nyumbani katika wiki chache zilizopita kujiandaa na kura ya maoni itakayoamua endapo eneo la Kusini lijitenge na kuwa taifa huru ama la.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR katika makambi ya wakimbizi wa ndani kwenye viunga vya Khartoum maelfu ya wakimbizi hao wanafungusha mizigo na wakisubiri kuondoka. Hata hivyo Adrian Edwards msemaji wa UNHCR anasema wakimbizi hao wanaorejea wanaongeza adha katika hali ya kibinadamu Sudan Kusini ambayo tayari inakabiliwa na changamoto ya kuwasaidia watu zaidi ya 215,000 walioathiriwa na mapigano ya kikabila, mashambulizi ya waasi na matatizo mengine ya kiusalama tangu Januari. Wanatumia usafiri wa aina mbalimbali ili mradi wafike.

(SAUTI YA ADRIAN EDWARDS)

Inakadiriwa wakimbizi wa ndani milioni mbili wamerejea nyumbani Sudan Kusini tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya amani 2005. Zimesalia siku chache tuu kabla ya kura ya maoni kufanyika nchini humo Januari 9 mwaka 2011.