Baraza la usalama limeongeza muda wa mpango wake Ivory Coast UNOCI

20 Disemba 2010

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limeongeza muda wa mpango wake wa kulinda amani nchini Ivory Coast UNOCI hadi Juni 30 2011.

Baraza limechukua uamuzi huo wakati mvutano wa kisiasa unaendelea nchini humo na Rais Laurent Gbagbo ametaka vikosi vya Umoja wa Mataifa na vya Ufaransa kuondoka nchini humo. Katika uamuazi huo wa pamoja bila kupingwa baraza limesema hali ya Ivory Coast inaendelea kuwa tishio kwa amani ya kimataifa na usalama wa eneo zima la Afrika ya Magharibi.

Baraza limeamua UNOCI itaendelea kuwa na walinda amani wake wote 8650 wakiwemo wanajeshi 7200 na waangalizi wa kijeshi 192. Pia baraza limempa idhini Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuongeza vikosi vingine 500 vitakavyohudumu hadi March mwakani.

Baraza limemtaka Ban na mwakilishi wake Ivory Coast kusaidia majadiliano nchini humo ili kuhakikisha amani na kuheshimiwa kwa matokeo ya uchaguzi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter