Wafuasi wa Gbagbo wanaendeleza ghasia dhidi ya UM: Choi

Wafuasi wa Gbagbo wanaendeleza ghasia dhidi ya UM: Choi

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu nchini Ivory Coast Young Jin Choi leo amesema kwamba hali ya usalama nchini humo bado ni tete.

Choi amesema mambo yalivyo sasa UNOCI inajikita katika masuala mawili muhimu ya jukumu lake, kwanza kuhalalisha uchaguzi na kuhakikisha amani iliwa ni pamoja na kuwalinda raia na hotel ya Golf anamoishi mgombea wa upinzani Alassane Ouattara.

Choi amesema kuanzia tarehe 15 mwezi huu wafuasi wa Rais Laurent Gbabgo aliyeshindwa kwenye uchaguzi na kukataa kuondoka madarakani wamekuwa wakiongeza vitendo vya ghasia dhidi ya jumuiya ya kimataifa, ikiwemo askari wa wanadiplomasia na mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNOCI.

UNOCI pia imesema mamia ya watu wametekwa tangu kufanyika kwa uchaguzi wa duru ya pili ya Urais mwezi uliopita. Watu hao wameelezewa kutwekwa kutoka majumbani kwao saa za usiku na kupelekwa kwenye mahabusu zilizo kinyume cha sheria ambako wanashikiliwa bila kuwa na mawasiliano yoyote na bila madai yoyote.

Kwa mujibu wa UNOCI utekaji huo unafanywa na watu wenye silaha na makundi ya wanamgambo wasiojulikana na watu wengine wamekutwa wamekufa katika mazingira ya kutatanisha.