Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM utatimiza wajibu wake Ivory Coast licha ya wito wa kutakiwa kuondoka: Ban

UM utatimiza wajibu wake Ivory Coast licha ya wito wa kutakiwa kuondoka: Ban

Umoja wa Mataifa utaendelea kutimiza wajibu wake katika nchi ya Afrika ya Magharibi ya Ivory Coast licha ya wito uliotolewa na Rais Laurent Gbagbo wa kutaka vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa UNOCI kuondoka nchini humo.

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa

Bwana Gbagbo alidai kushinda uchaguzi mkuu wa Uraia uliofanyika mwezi uliopita ,lakini jumuiya ya kimataifa kwa pamoja imesema kwamba kiongozi wa upinzani, Alassane Outtara alishinda na ndiye anayetakiwa kua Rais.

Katika taarifa maalumu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNOCI,utatimiza wajibu wake na utaendelea kuangalia ukiukaji wowote wa haki za binadamu na ghasia, pia mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Jana Jumamosi wanajeshi wawili wa Umoja wa Mataifa walijeruhiwa baada ya kushambuliwa na majeshi ya serikali ya Ivory Coast yanayomuunga mkono bwana Gbagbo. Ban ameongeza kuwa kutakuwa na athari kwa wale wote wanaojihusisha na mashambulizi dhidi ya majeshi ya Umoja wa Mataifa.