Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amtaka Laurent Gbagbo kuachia ngazi

Ban amtaka Laurent Gbagbo kuachia ngazi

Rais Laurent Gbagbo wa Ivory Coast ametakiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuachia ngazi na kuruhusu mpinzani wake aliyechaguliwa kushika hatamu.

Bwana Gbagbo amekataa kukubali kushindwa dhidi ya Rais aliyechaguliwa Alassane Ouattara kwenye duru ya pili ya uchaguzi uliofanyika mwezi ulipita. Ban amesema jaribio lolote la kuidhibiti hoteli ya Golf mjini Abijan ambayo inatumika kama makao makuu ya bwana Ouattara au kuzuia operesheni za mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo halikubaliki.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

"Kulikuwa na mshindi dhahiri, kushirikiana madaraka sio chaguo. Juhudi za Laurent  Gbagbo  na wafuasi wake kun'gang'ania madaraka na kukiuka matakwa ya umma hazitaruhusiwa kufanyika. Nnamtaka aachie madaraka na kuruhusu mrithi wake aliyechaguliwa kuchukua majukumu bila vikwazo zaidi. Jumuiya ya kimataifa lazima ipeleke ujumbe huu waziwazi. Matokeo mengine yoyote ni dhihaka kwa demokrasia na utawala wa sheria."