Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya Waivory Coast wakimbilia nchi jirani:UNHCR

Maelfu ya Waivory Coast wakimbilia nchi jirani:UNHCR

Wakimbizi kutoka Ivory Coast wanakimbilia nchi jirani ya Liberia kwa idadi ya watu 150 kwa siku katika wakati huu ambapo mvutano wa kisiasa bado unaendelea nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, mgogoro wa Ivory Coast umesababishwa na Rais aliyekuwa mpiganaji Laurent Bagbo kutoafiki matokeo ya uchaguzi, kukubali kushindwa na kumtambua mpinzani wake Alassane Outtara kama mshindi kwenye duru ya pili ya uchaguzi wa uraisi.

Msemaji wa UNHCR Adrian Edward anasema timu ya shirika hilo hivi sasa inawandikisha na kuwasaidia wakimbizi hao wa Ivory Coast wanaowasili Liberia. Ameongeza kuwa tangu Jumamosi wiki iliyopita takribani watu 3500 wameingia Liberia huku kukiwa na taarifa kutoka katika vijiji mbalimbali vya mpakani kuwa watu wapatao 150 wanaingia kila siku.

Kwa ushirikiano na serikali ya Liberia watu wanapata hifadhi kwenye jamii, wanakijiji wamewapokea katika nyumba zao na wanashirikiana nao kwa kila hali. Wakati huohuo kuna taarifa ya watu wengine kutoka Ivory Coast kukimbilia Guinea, hadi sasa waliorodheshwa na UNHCR ni 200 ingawa kuna ripoti kwamba wakimbizi zaidi wamewasili Jumatatu wiki hii katika mji wa Lola.