Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF ni mfuko muhimu kwa kuokoa maisha ya watu:Ban

CERF ni mfuko muhimu kwa kuokoa maisha ya watu:Ban

Mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF ni muhimu sana na ni chombo kinachoongoza duniani kutoa msaada wakati wa majanga amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Akizungumza kwenye mkutano maalumu katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa hii leo kuhusu mfuko huo Ban amesema mara nyingi unachukua hatua haraka, unawajibika na kubwa zaidi unaokoa maisha ya watu.

Amesema miaka mitano tangu ulipoanzishwa na baraza kuu la Umoja wa Mataifa CERF umekuwa sehemu ya msaada wa kibinadamu kwa kutoa fedha haraka na kuyaruhusu mashirika ya misaada kutekeleza wajibu wao panapozuka matatizo.

Hadi sasa mfuko huo amesema umeshatoa dola karibu bilioni 1.8 kuwasaidia mamilioni ya watu wanaohitaji msaada. Kwa mwaka huu pekee nchi 44 duniani zimetumia takribani dola milioni 400 kutoka mfuko wa CERF kupata huduma muhimu kama chakula, malazi, madawa, maji na vifaa vingine. Miongoni mwa nchi zilizosaidiwa mwaka huu ni Haiti, Pakistan, nchi za eneo la Sahel, Somalia, Nigeria ,Jamhuri ya Afrika ya Kati, Madagascar, Georgia, Djibouti na Mongolia. Ban amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyoletwa na mfuko huo, CERF ni lazima ifikie matarajio ya nchi wanachama, na muhimu zaidi lazima iwasaidie walioathirika zaidi wakati wa majanga kwani huo ndio mtihani mkubwa wa uwajibukaji wa mfuko huo.