Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa Haki za Binadamu wa UM wahofia kusumbuliwa kwa watetezi wa haki Uchina

Wataalamu wa Haki za Binadamu wa UM wahofia kusumbuliwa kwa watetezi wa haki Uchina

Wataalamu watatu wa haki za binadamu wameelezea hofu yao dhidi ya kusumbuliwa na kukamatwa kwa watetezi wa haki za binadamu nchini Uchina tangu kutangazwa kupewa tuzo ya Nobel kwa mpigania haki Liu Xiaobo miezi miwili iliyopita.

Wataalamu hao wamesema tangu tarehe 8 Oktoba 2010, wamepokea taarifa za kukamatwa au kuwekwa rumande kwa zaidi ya watetezi 20 wa haki za binadamu na wengine zaidi ya 120 kuwekwa kwenye vifungo vya nyumbani, akiwemo mke wa Liu Xiaobo bi Liu Xia. Hatua zingine zinazochukuliwa ni pamoja na vikwazo vya usafiri, kuhamishwa kwa lazima, kupewa vitisho na kufungiwa njia za mawasiliano kupitia mtandao hasa kwa masuala yoyote yanayohusu tuzo ya amani ya Nobel.

Wataalamu hao mwakilishi maalumu katika kutetea haki za binadamu Margaret Sekaggya, mwakilishi maalumu katika kuchagiza na kutetea haki na uhuru wa maoni na wa kujieleza Frank La Rue na mwenyekiti wa kundi linaloangalia masuala ya kuwekwa mahabusu El Hadji Malick Sow, wamesisitiza kwamba hali hiyo inayoendelea nchini Uchina inawafanya kuhoji jukumu la nchi hiyo katika kuchagiza na kulinda haki za kimataifa za binadamu na wameitaka Uchina kumwachilia mpigania haki Liu Xiaobo.