Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2010 umevunja rekodi ya joto:WMO

Mwaka 2010 umevunja rekodi ya joto:WMO

Mwaka huu bila shaka unatarajiwa kushika rekodi ya miongoni mwa miaka mitatu iliyowahi kuwa na joto sana duniani tangu kuanzishwa kwa chomo ya kuweka takwimu za hali ya hewa mwaka 1850, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa duniani WMO.

Kiwango cha pamoja cha joto kwa bahari na nchi kavu kati ya Januari hadi Oktoba mwaka huu kinakadiriwa kuwa nyuzi joto 55 zaidi ya kile cha mwaka 1961 hadi 1990 ambacho kwa wastani kilikuwa nyuzi joto 14. Hivi sasa hali ya joto kwa mwaka huu imevunja rekodi ya juu iliyowekwa kati ya Januari hadi Oktoba 1998 iliyokuwa nyuzi joto 53 na ile ya 2005 iliyokuwa nyuzi joto 52. George Njogopa na taarifa kamili.

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mwaka huu unatarajiwa kuwa miongoni mwa miaka mitatu iliyoshuhudia joto zaidi tangu ilipoanza kurikodiwa mwaka 1850, suala linaloonyesha mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na mwanadamu.  Ripoti iliyotolewa na jopo la wataalamu wanaohudhiria mkutano unaofanyika Cancun Mexico, kwa lengo la kujaribu kuzuia kuongezeka joto la dunia, hali inaonyesha kuwa kadiri siku zinavyokwenda ndivyo joto la dunia linavyoongezeka.

Hata hivyo imeelezwa kuwa endapo kutashuhudiwa baridi mwezi huu wa Disemba hali hiyo ya joto inaweza isishuhudiwe. Mkutano wa Cancun unajaribu kutafuta muafaka kuhusiana na makubaliano ya mkutano wa mwaka ujao wa Copenhagen juu ya kupunguza ongezeko la joto kwa nyuzi 2.  Hii ni katika hali ambayo kiwango kilichoahidiwa na Marekani na China cha kupunguza gesi zinazochafua mazingira ili kufikiwa lengo hilo kikiwa kidogo sana.