Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OSCE imetakiwa kusaidia kipindi cha mpito Afghanistan

OSCE imetakiwa kusaidia kipindi cha mpito Afghanistan

Shirika kwa ajili ya usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE limetakiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kusaidia kuhakikisha kwamba kipindi cha mpito kuelekea demokrasia nchini Afghanistan kinadumu na kuwezekana.

Akizungumza kwenye mkutano wa OSCE mjini Astana Kazakhstan Ban amesema hali ya Afghanistan ni mtihani kwa ushirikiano wa kimataifa. Katibu Mkuu ametoa wito msaada wa muda mrefu wa kuwapa mafunzo watu wa Afghanistan na kujenga taasisi zao.

Amesema Umoja wa Mataifa utakaribisha ushiriki mkubwa wa OSCE katika kusaidia mipango ya kitaifa ya Afghanistan. Kwa upande wa Umoja wa Mataifa tunapanga kuzindua programu ya kikanda kwa ajili ya Afghanistan na nchi jirani mapema mwakani.

Mipango hiyo itahusisha ushirikiano wa mipakani ili kukabiliana na tishio la karne ya 21 la usafirishaji haramu wa mihadarati na uhalifu wa kupangwa.