Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamhuri ya Afrika ya Kati mkamateni Rais Bashir:ICC

Jamhuri ya Afrika ya Kati mkamateni Rais Bashir:ICC

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC leo imeiomba Jamhuri ya Afrika ya Kati kuchukua hatua zote muhimu ili kumkamata Rais wa Sudan Omar Al-Bashiri na kumpeleka kwenye mahakama hiyo wakati atakapowasili nchini humo.

ICC mwezi Julai mwaka huu ilitoa kibali kingine cha kukamatwa Rais Bashir ikiongeza kosa la mauaji ya kimbari katika mashitaka yanayomkabili ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwenye jimbo la Darfur.

Ombi la leo la ICC limefuatia taarifa kwamba kuna uwezekano kwamba Rais Bashir atazuru nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mahakama hiyo imesisitiza kwamba kama mmoja ya waliotia sanini mkataba wa Roma Jamhuri ya Afrika ya Kati ina wajibu wa kumkamata Rais Bashir akizuru nchini humo. Mkataba wa Roma ulianzishwa na ICC na kuanza kutekelezwa Julai mosi mwaka 2002.