Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR imeitaka Uswis kutorejesha waomba hifadhi

UNHCR imeitaka Uswis kutorejesha waomba hifadhi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo limeiomba serikali ya Uswis kuhakikisha kwamba sheria za kutowarejesha kwa nguvu waomba hifadhi haziko hatarini hasa wakati huu ambapo kuna mjadala unaendelea wa kuwafukuza wageni ambao ni wahalifu.

Shirika hilo limesema kutowarejesha kwa nguvu wakimbizi na wanaoomba hifadhi ni moja ya sheria za kimataifa na imewekwa kuhakikisha kwamba hakuna muomba hifadhi hata mmoja anayerejeshwa kwenye hali ambayo anaweza kukabiliwa na matatizo makubwa kama kuuawa, kuteswa, kunyanyaswa na kufanyiwa vitendo vingine visivyo vya kibinadamu.

UNHCR inasema kwa mfumo wowote wa kuomba hifadhi kuweza kufanya kazi ipasavyo matatizo binafsi lazima yasikilizwe na msaada wa kisheria utolewe badala ya kuwarejesha makwao ambako maisha yao yatakuwa hatarini.

Kwa mujibu wa shirika hilo Switzerland imetia saini mkataba wa wakimbizi wa mwaka 1951 na mingine inayohusiana na haki za binadamu hivyo ni lazima iheshimu mikataba hiyo.