Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika iko hatarini kupoteza vyanzo vya maji:UNEP

Afrika iko hatarini kupoteza vyanzo vya maji:UNEP

Utafiti mpya ulioangazia hali ya upatikanaji wa maji safi ya kunywa umetaja changamoto zinazozikabili nchi nyingi za afrika kushindwa kusambaza maji kwenye maeneo mbalimbali.

Utafiti huo uliofanywa na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulika na mazingira UNEP,umetaja kuwa sababu mojawapo ni ile inayotokana na kuanza kutoweka kwa uasili wa vyanzo kadhaa vya maji ikiwemo kukauka kwa ziwa Chad, na kumomonyoka kwa sehemu ya ukanda wa mto Nile.

Ripoti hiyo imeelezea wasiwasi wake hasa kutokana na kuanza kupungua kwa kiwango cha upatikanaji maji kwa kila raia barani afrika. Aidha ripoti hiyo imesema kuwa kumekuwa na madhara makubwa kwa baadhi ya maeneo ikiwemo nchini Uganda kuanguka kwa shughuli za kilimo na kuwepo kwa hewa chafu kwenye baadhi ya maeneo nchini Nigeria.

Wasiwasi mkubwa ni kwamba iwapo hali hiyo itaendelea, basi huenda nchi nyingi za afrika zikashindwa kufikia shabaya ya moja ya malengo ya maendeleo ya mellenia ambayo yanataka ifikapo mwaka 2015 nusu ya wakazi wanaondokana na shida ya kukosa maji safi ya kunywa.