UM umelaani vikali shambulio la Korea Kaskazini:Ban

23 Novemba 2010

Shambulio la leo la makombora lililofanywa na Korea ya Kaskazini kwenye kisiwa cha Yeongpyeong Korea Kusini limelaaniwa vikali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Katika taarifa yake iliyowasilishwa na msemaji wake hii leo Ban amesema amesikitishwa na kupotea kwa maisha ya watu na kutoa salamu za pole kwa waathirika na familia zao.

Ban amesema anahofia kuendelea kwa hali ya mvutano kwenye rasi ya Korea na kuelezea shambulio la Korea ya Kaskazini kama moja ya matukio mabaya tangu kumalizika kwa vita vya Korea mwaka 1953.

Ban ametoa wito wa kusitisha mara moja mashambulizi na kusisitiza kwamba tofauti zozote zilizopo zitatuliwe kwa njia ya amani na mazungumzo. Katibu Mkuu amemweleza Rais wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hofu yake juu ya hali hiyo ya Korea.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter