Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji katika sekta ya kilimo lazima ukuwe:FAO

Uwekezaji katika sekta ya kilimo lazima ukuwe:FAO

Mkurugenzi mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani FAO Jacques Diouf leo amesema hakikisho la kukabili matatizo ya muda mrefu ya chakula duniani ni kuwekeza katika kilimo.

Amesema ongezeko la njaa na utapia mlo tangu kuzuka kwa matatizo makubwa ya chakula 2008 yanadhihirisha upungufu katika mfumo wa kimataifa wa chakula na haja ya haraka ya kufanya mabadiliko. Diouf ameyasema hayo akihutubia kungamano la baraza la mawaziri la ushirikiano wa nchi za Ghuba na uwekezaji wa kilimo Abu Dhabi.

Kongamano hilo limehudhuriwa na wawakilishi kutoka Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia na wenyeji Muungano wan chi za Falme za Kiarabu UAE. Jayson Nyakundi na taarifa zaidi.

(RIPOTI YA JAYSON NYAKUNDI)

Kupanda kwa bei ya vyakula na hali ya mbaya ya uchumi duniani vyote vimezua madharamakubwa kwa mamilioni ya watu sehemu zote za ulimwengu. Hii ni baada ya bei ya bidhaa nyingi za kilimo kupanda na kukaribia kuweka rekodi mwaka huu wa 2010 tangu kuanza kushuhudiwa kupanda kwa bei ya vyakula mwaka 2008.

Hali hii huenda sasa ikawa changamoto kubwa kwa nchi za ghuba ambazo zinategemea kwa asilimia kubwa ununuzi wa chakula kwa wananchi wao. Katika sehemu za mashariki na kaskazini mwa Afrika idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa na utapiamlo imefikia watu milioni 37 ambayo ni karibu asilimia 10 ya wakaazi wote wa maeneo hayo.