Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi wa mashambani ndio waathirika wa HIV:IOM

Wafanyakazi wa mashambani ndio waathirika wa HIV:IOM

Ripoti mpya ya shirika la kimataifa la uhamiaji IOM inasema maambukizi ya virusi vya HIV ni ya juu miongoni mwa wafanyakazi wa mashambani nchini Afrika ya Kusini.

Utafiti wa ripoti hiyo umebaini kwamba wafanyakazi wa mashambani kwenye majimbo ya Limpopo na Mpumalanga ndio yaliyo na kiwango cha juu cha maambukizi kwa wafanyakazi wa mashambani kuliko majimbo mengine ya Afrika ya Kusini.

Utafiti huo umefanyika kwenye mashamba 23 makubwa ya biashara maeneo ya Malelane, Musina na Tzaneen na kuhusisha wafanyakazi 2810. George Njogopa na taarifa kamili.

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Utafiti huo ambao umefanyika kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia March hadi May mwaka huu, unaonyesha kuwa maambukizi hayo yameenea zaidi katika majimbo ya Limpopo na Mpumalanga. Kwa mfano katika utafiti wake, kuligundulika kuwa asilimia ya 39.5 ya wafanyakazi hao waliopimwa waligundulika kuwa na virusi vya ugonjwa wa UKIMWI, kiwango ambacho ni mara dufu ya kile kilichotolewa na shirika la umoja wa mataifa linalohusika na masuala ya UKIMWI UNAIDS.

Ili kukabiliana na hali hiyo, ripoti ya utafiti huo imeanisha mapendekezo kadhaa ikiwemo kuwasogezea huduma za kiafya wafanyakazi hao na bila kuweka kando mikakati ya kuongeza elimu ya ufahamu miongoni mwao.