Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maambukizi mapya ya virusi vya HIV na ukimwi yanapungua duniani:UNAIDS

Maambukizi mapya ya virusi vya HIV na ukimwi yanapungua duniani:UNAIDS

Idadi ya watu wapya wanaoambukizwa virusi vya HIV na ukimwi inapungua kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na mpango wa pamoja kupambana na ukimwi wa Umoja wa Mataifa UNAIDS.

Watu takribani milioni 2.6 waliambukizwa virusi vya HIV mwaka 2009 idadi ambayo ni ndogo kwa asilimia 20 ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita. UNAIDS inasema hali hiyo inaambatana pia na kupungua kwa vifo vitokanavyo na maradhi yanayohusiana na ukimwi ambayo kwa mwaka jana wa 2009 vilikuwa milioni 1.8 ikilinganishwa na vifo milioni 2.1 mwaka 2004.

Mkurugenzi mkuu wa UNAIDS Michel Sidibe anasema uwekezaji katika kukinga na mipango ya tiba unazaa matunda, lakini juhudi zaidi zinahitajika.

(SAUTI YA MICHEL SIDIBE)

UNAIDS inasema ufadhili wa kimataifa wa mipango ya tiba na kinga kwa virusi vya HIV na ukimwi unapungua na usipoangaliwa kwa makini basi unaweza kugeuza mafanikio yaliyoaanza kupatikana.