Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS yakaribisha tamko la Papa kuhusu Condom

UNAIDS yakaribisha tamko la Papa kuhusu Condom

Shirika la Umoja wa mataifa linalopambana na maradhi ya ukimwi UNAIDS limekaribisha matamshi ya baba Benedict wa kumi na sita kuwa matumizi ya mipira ya kondomu kuzuia maambukizi ya ukimwi yanakubalika .

Mkurugenzi wa UNAIDS Michel Sidibe ameyataja matamshi hayo kama mwelekeo mwema uliochukuliwa na makao ya Vatican akiongeza kuwa hiyo ni moja ya njia ya kutambua matumizi ya kondomu na wajibu muhimu katika kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa ukimiwi.

Sidibe amesema kuwa UNAIDS imekuwa ikishirikiana kwa karibu na makao ya Vatican na kufanya majadiliano na maaskofu wa kanisa hilo kuhusu masuala ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto , kuwakinga vijana dhidi ya maambukizi na kupunguza dhuluma za kimapenzi miongoni mwa akina mama na watoto wasichana.

Huku kukiripotiwa maambukizi 7000 ya ugonjwa wa ukimwi kila siku UNAIDS inatoa wito wa kutumika njia za kuzuia maambukizi hayo zikiwemo matumizi ya mipira ya kondomu , kutokuwa na wapenzi wengi , tohara za wanaume miongoni mwa zingine.