Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 2 kuchanjwa polio Uganda:WHO/UNICEF

Watoto milioni 2 kuchanjwa polio Uganda:WHO/UNICEF

Katika hatua za kukabiliana na visa vya polio vilivyobainika kwenye wilaya ya Bugiri nchini Uganda, wizara ya afya ya nchi hiyo, shirika la afya duniani WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wanaanza duri ya kwanza ya chanjo nchini humo.

Chanjo hiyo itakayoanza Jumamosi Novemba 20 hadi 22 itawalenga watoto milioni mbili walio na umri wa chini ya miaka mitano katika wilaya 48 mashariki, Kaskazini mashariki na Kaskazini mwa Uganda.

Waziri wa afya wa Uganda Dr Stephen Mallinga amesema watajitahidi kudhibiti ugonjwa huo ili Uganda itangaze tena kuwa huru bila polio.

Polio ni ugonjwa unaoambukiza na unasambaa haraka kwa wasio na kinga hususan watoto. Ugonjwa huu unasababisha kupooza na wakati mwingine vifo, licha ya kwamba hauna tiba lakini kusambaa kwake kunaweza kuzuiwa kwa njia ya chanjo.

Wafanyakazi wa afya kuanzia kesho watapita nyumba hadi nyumba kwenye maeneo yanayoelengwa ili kuhakikisha kila motto wa chini ya umri wa miaka mitano anapata chanjo. Duruy a pili ya chanjo hiyo itafanyika December 11-13 mwaka huu na ya mwisho Januari 15-17 2011.