Skip to main content

Afrika iongeze ushindani katika maendeleo ya viwanda:Ban

Afrika iongeze ushindani katika maendeleo ya viwanda:Ban

Tarehe 20 ya kila November ni siku ya maendeleo ya viwanda Afrika, na mwaka huu imeangukia wakati ambao dunia inakabiliwa na msukosuko mkubwa wa kiuchumi.

Msukosuko huo umeligusa pia bara la Afrika japo sio kwa kiasi kikubwa sana. Katika ujumbe maalumu wa kuadhimisha siku hiyo ambayo kauli mbulu yake mwaka huu ni ushindani wa viwanda kwa maendeleo ya Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-moon amesema bidhaa zinazozalishwa Afrika kwa mwaka 2008 zilikuwa ni asilimia 0.9 ya bidhaa zote duniani na bidhaa inazoingiza ni zaidi ya nusu ya inazosafirisha nje.

Amesema kuna haja ya kuongeza ushirikiano wa kimataifa ili umuhimu na uwezo wa bara hilo uonekane.Amesema kilimo na madini ya Afrika yanaweza kuleta matunda mazuri kwa bara hilo hasa kwenye uchumi wa dunia na changamoto ni kulisaidia bara hilo kujenga uwezo wake katika maeneo hayo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la viwanda UNIDO linaendelea kusaidia utekelezaji wa mikakati ya muungano wa Afrika ya kuchagiza ukuaji wa viwanda barani humo. Lakini mafanikio yatategemeana na rasilimali zitokazo Afrika na washirika wao. Kukusanya rasilimali hizo na kuzitumia vizuri ni muhimu sana hasa katika kipindi hiki cha matatizo ya kimataifa ya uchumi ambapo mahitaji ya bidhaa zitokazo Afrika yamepungua.

Ban amesema Afrika sio bara pekee lililoathirika lakini mtazamo endelevu wa maendeleo unaweza kusaidia kuziinua jamii za Afrika, kulinda mazingira na kutoa mchango mkubwa katika kuwa na maisha bora kwa wote.