Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada kwa mfuko wa kusaidia waathirika wa usafirishaji haramu watu waongezeka

Msaada kwa mfuko wa kusaidia waathirika wa usafirishaji haramu watu waongezeka

Mfuko mpya ulioanzishwa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa kusaidia waathirika usafirishaji haramu wa watu unaendelea kupata ongezeko la msaada wa kimataifa.

Msaada huo ni pamoja na ahadi kutoka nchi sita na muhisani mmoja binafsi katika kipindi cha wiki mbili zilizopita kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uhalifu na madawa UNOCD. Yury Fedotov, mkurugenzi mtendaji wa UNODC amesisitiza kwamba mfuko huo ambao ni wa hiyari kuwasaidia waathirika wa usafirishaji haramu wa watu utafanikiwa tuu ukipata msaada unaohitajika wa kifedha.

Amezichagiza serikali zote, wahisani, sekta binafsi na watu binafsi kuchangia katika mfuko huo.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba watu milioni 2.4 wananyonywa na kudhulumiwa baada ya kusafirishwa kiharamu na magenge ya wahalifu. Fedetov amesema na wananyonywa kwa njia mbalimbali ikiwemo utumwa wa ngono ambao ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Mfuko huo utatoa msaada wa kibinadamu, kisheria na kifedha kupitia vitengo vya misaada vilivyoandaliwa kama serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na jumuiya za kijamii. Mfuko huo ulizinduliwa rasmi November 4 baada ya kupitishwa na baraza kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Julai.