Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waasi Darfur watakiwa kujiunga na machakato wa amani:UM

Waasi Darfur watakiwa kujiunga na machakato wa amani:UM

Makundi ya waasi kwenye jimbo la Darfur Sudan yametakiwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kujiunga na mchakato wa amani ili kupata suluhisho la kudumu la mgogoro wa nchi hiyo.

Baraza la usalama limeelezea hofu yake kuhusu ongezeko la ghasia na usalama mdogo kwenye jimbo la Darfur ikiwemo mashambulizi ya makundi ya waasi na makombora yanayovurumishwa kwa njia ya anga na majeshi ya serikali ya Sudan.

Baraza limesema bado lina msimamo wa kusaidia mchakato wa amani ya Darfur unaoongozwa na muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwa msaada mkubwa pia wa mwenyeji wa mazungumzo serikali ya Qatar. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague ameyasema hayo kwqenye mkutano wa baraza la usalama uliofanyika leo mjini New York kuhusu Sudan.

Amesema baraza linayataka makundi yote ya waasi kujiunga na mchakato wa amani bila kuchelewa na bila vikwazo vyoyote , na pande zote zisitishe mapigano mara moja. Ameongeza kuwa baraza pia limezitaka pande zote kujihusisha na majadiliano kwa mtazamo wa kutafuta suluhu na amani ya kudumua ya Darfur.