Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ikipata msaada Afrika itatimiza malengo ya milenia:Migiro

Ikipata msaada Afrika itatimiza malengo ya milenia:Migiro

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha-Rose Migiro amesema kuwa kutokana na utajiri mkubwa ulio barani Afrika bara la Afrika linaweza kutimiza malengo ya milennia ifikapo mwaka 2015.

Akiyahutubia mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotoa huduma zao barani Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia bi Migiro amesema kuwa Afrika inahitaji uungwaji mkono wa kimataifa. Amesema kuwa kile wenyeji wa bara hilo wanahitaji ni njia za kujipatia mapato na nafasi za ajira.

Amesema kuwa athari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa na changamoto zikiwemo za kiuchumi , chakula na kawi vinaendelea kuwa kizingiti cha maendeleo barani afrika na vinayaweka hatarini mafanikio ya kimaendeleo yaliyopatikana.

Bi Migiro ameongeza kuwa kuwa hata baada ya kuwepo kwa changamoto nyingi uchumi wa bara la Afrika unaendekea kukua ambapo unakadiriwa kukua kwa asilimia 4.8 mwaka huu wa 2010 kutokana na mauzo ya madini na serikali kuelekeza asilimia kubwa ya bajeti zao kwa maendeleo ya miundo mbinu.