Mataifa yanayochipuka yapiga hatua katika utafiti:UM
Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa mataifa yanayoinukia kichumi yanaendelea kupunguza mwanya wa utafiti wa kisanyansi na maendeleo uliopo katika ya nchi zilizostawi na zile zinazoendelea wakati China , India na Korea zikiwekeza zaidi kwenye masuala ya Sayansi na Teknolojia.
Ripoti hiyo ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , Sayansi na utamaduni UNESCO inasema kuwa ufadhili kwenye sekta za utafiti na maendeleo barani Asia uliongezeka kutoka asilimia 27 hadi 32 katia ya mwaka 2002 na 2007 huku ufadhili huo ukipungua barani Ulaya , Marekani na nchini Japan.
Ripoti hiyo iliyotolewa sambamba na maadhimisho ya siku ya sayansi duniani kwa amani na maendeleo inaonyesha kuwa takriban asilimia 83 ya utafiti na maendeleo ulifanyika kwenye nchi zilizostawi mwaka 2002 lakini mwaka 2007 utafiti huo ulipungua hadi asilimia 76.