Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO imezindua ripoti ya udhibiti wa TB 2010

WHO imezindua ripoti ya udhibiti wa TB 2010

Shirika la afya duniani WHO leo limezindua ripoti muhimu kabisa kuwahi kutolewa kuhusu hatua zilizopigwa kukabiliana na ugonjwa wa kifua kikuu (TB) 2010.

Ripoti hiyo ina takwimu mpya kabisa na kwa mara ya kwanza imejumuisha makusanyo ya kwenye mtandao wa kompyuta kutoka nchi na mataifa 212 duniani. Matokeo ya ripoti hiyo yanathibitisha kwamba kukiwepo na mipamo bora ya WHO, fedha zinazohitajika na serikali kutimiza wajibu wao basi ugonjwa wa kifua kikuu unaweza kudhibitiwa.

Dr Mario Raviglione mkurugenzi wa WHO kitengo cha kukomesha TB anasema wameshuhudia hatua nzuri zimepigwa katika huduma kwa walio na kifua kikuu na amesema hatua hizo zimekuwa na athari nzuri kwa nchi masikini.

Tangu mwaka 1995 watu milioni 41 wameponywa na maisha ya watu milioni 6 yameokolewa kutoka kwa ugonjwa huo, Dr Mario anasema haya ni mafanikio makubwa na sio miujiza, hata hivyo amesema bado watu milioni 1.7 hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huo wakiwemo wanawake 380,000, amesema bado nchi nyingi hazifanyi juhudi za kutosha hivyo ni lazima zitumie kila fursa iliyopo kuvishinda vita hivi.