Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wapongeza duru ya pili ya uchaguzi Guinea:Djinnit

UM wapongeza duru ya pili ya uchaguzi Guinea:Djinnit

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa huko Afrika ya Magharibi ameipongeza Guinea kwa kufanya duru ya pili ya uchaguzi wa urais kwa amani, akisema kuwa wananchi wa eneo hilo wamedhihirisha namna wanavyowajibika kuenzi demokrasia kwa kushiriki kwenye upigaji kura.

Said Djinnit amesema kufanikiwa kwa uchaguzi huo ni ishara inayotolewa na wananchi hao namna walivyotayari kulivusha taifa lao na kulifikisha pahala ambalo utawala wa katiba na sheria unazingatiwa.

Hata hivyo amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu kabla na baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, na wakati huo huo amewataka wagombea wa nafasi hiyo Cellou Dalein Diallo na Alpha Condé kudhibitisha kwa vitendo kile walichokihadi hapo kabla kuwa watakuwa tayari kuheshimu sheria ili kuepusha matukio ya ghasia.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na shirika la habari la Umoja wa Mataifa, Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa ni dhamira ya Umoja wa Mataifa kuona kwamba demokrasia ya kweli inapatikana kwa amani na utulivu.