Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji ya Ethiopia na Somalia waokolewa ghuba ya Aden

Wahamiaji ya Ethiopia na Somalia waokolewa ghuba ya Aden

Kundi la wahamiaji 62 waliookolewa na meli ya jeshi ya Marekani katika ghuba ya Aden wamesafirishwa na shirika la kimataifa la uhamiaji IOM hadi kwenye kambi ya wakimbizi nchini Kenya.

Wahamiaji hao ambao ni Waethiopia na Wasomali walikuwa njiani kuelekea Yemen zaidi ya mwezi mmoja uliopita wakati boti yao ilipopata matatizo ya kiufundi na wakalazimika kuelea majini kwa siku nane. Ingawa walitoa taarifa ya kupatwa na tatizo lakini imeelezwa kuwa baadhi yao waliamua kujitosa majini kumaliza adha zilizokuwa zinawakabili za ukosefu wa chakula na maji.

Meli ya kijeshi ya Marekani ikaenda kuwaokoa lakini tayari wengine 38 walikuwa wameshafariki dunia njiani. IOM ikawachukua walionusurika na kuwapeleka kwenye kambi ya wakimbizi baada ya serikali ya Kenya kukubali kuwapokea. Wahamiaji hao 62, 53 kati yao ni Waethiopia na tisa Wasomali, na miongoni mwao kulikuwa na wanawake 12 na watoto 2 waliokuwa bila mwangalizi.